KIKOSI chetu kimefanya mazoezi ya kwanza ya ufundi asubuhi ya leo kwenye viwanja vya Olympic de Rades hapa Tunis, Tunisia.

Mazoezi haya yaliodumu kwa saa moja na nusu yalianza saa 10:30 kwa saa za hapa Tunisia [Sawa na saa 12:30 mchana kwa Tanzania].

Akizungumza na YANGA MEDIA kocha msaidizi wa Yanga, Cedric Kaze alisema, wao kama benchi la ufundi wanafurahishwa na maandalizi mazuri yaliyofanywa na uongozi wa Yanga kuelekea mchezo wa Jumapili, dhidi ya Monastir ya Tunisia.

“Leo tumefanya mazoezi ya pili hapa Tunisia, jana tulianza na recovery na leo tumekuja uwanjani. Kila kitu mpaka sasa kiko sawa na wachezaji wanaonyesha kuwa na furaha na kujituma sana,” alisema Kaze.

Wachezaji wote 24 walihudhuria mazoezi haya yaliyosimamiwa na kocha mkuu, Nasredine Nabi kasoro golikipa Aboutwaleb Mshery aliyesafiri kwenda Sousse kwa ajili ya matibabu.