KIVUTIO kikubwa kwa mashabiki wa soka katika mchezo wa Ligi Kuu kati ya Yanga na Namungo FC ni goli lililofungwa na Dickson Job.

Goli hili la kwanza kwa Yanga kwenye mchezo huu lilifungwa kwa kichwa kikali na Job akiunganisha vyema kona iliyopigwa na Djuma Shabani dakika ya 43.

Sasa pengine umekuwa ukijiuliza, hili ni goli la ngapi kwa Job kulifunga tangu ajiunge na Yanga misimu miwili iliyopita? Ni goli la ngapi pia tangu aanze soka?

Majibu ni kwamba, goli alilofunga Job kwenye mchezo wa Namungo, ni goli lake la kwanza kabisa tangu atue Yanga.

Na kwenye maisha yake ya soka, ni goli lake la pili ndani ya dakika 90. Goli lake la kwanza kabisa alilifunga kwenye mchezo wa timu ya Taifa ya Tanzania dhidi ya Somalia.

Lakini hili goli dhidi ya Somalia, alilifunga kwa mkwaju wa penalti. Na hapa Dickson Job anatueleza umahiri wake kwenye kupiga penalti ulivyo.

“Mimi ni mtaalam sana wa penalti, ndani ya dakika 90 nimefunga moja dhidi ya Somalia Lakini nina magoli mengine ya penalti niliyofunga kwenye zile penalti tani tano.

“Hili goli dhidi ya Namungo ndio goli la kwanza kabisa kwangu kufunga kwa kichwa na Nimefurahi sana,” alisema Dickson Job