Uongozi wa Klabu ya Yanga unasikitishwa na tamko lililotolewa na Mdhamini wetu mkuu ‘SportPesa’ likiishutumu Klabu ya Yanga kukiuka makubaliano ya kimkataba kwa kuzindua jezi maalumu ya mashindano ya Kombe la Shirikisho la CAF yenye nembo ya Mdhamini mwingine “Haier”.

Klabu inapenda kuutarifu umma kwamba, inatambua na itaendelea kuitambua “SportPesa” kama Mdhamini mkuu na itaendelea kuheshimu vigezo na masharti vilivyoainishwa kwenye mkataba.

Hivyo basi, ni muhimu kuelewa kuwa haki ya SportPesa kwenye nafasi ya mbele ya jezi sio haki isiyo na mipaka “absolute rights” kama ilivyoelezwa kwenye tamko la SportPesa.  Haki yao ina mipaka kulingana na sheria na kanuni za mashindano ambayo klabu ya Yanga inashiriki. Yanga inaendeshwa kwa kufuata sheria na kanuni za TFF, CAF na FIFA ambazo ziko juu ya makubaliano binafsi ambayo klabu inaweza kuyaingia na wadau mbalimbali ikiwemo SportPesa.

Muongozo wa CAF kuhusiana na klabu zinazoshiriki mashindano ya Kombe la Shirikisho la CAF kwenye hatua ya makundi unazuia matumizi ya udhamini wa kampuni za michezo ya ubashiri “Betting”.

Uongozi wa Yanga uliwajulisha SportPesa juu ya matumizi ya nembo ya Haier, kama mbadala wa udhamini kwenye mashindano ya CAF. Taarifa hiyo ilizua mjadala, ingawa mjadala huo haukuwa na mashiko kwenye mkataba.

Mnamo Januari 27, 2023 SportPesa waliiandikia Klabu ya Yanga juu ya matumizi ya nembo mbadala ya “SpScore.com” ambayo inasimama badala ya “SportPesa Score”,  nembo hii ilikataliwa na CAF kwa msingi uleule kuwa ni mshirika na SportPesa.

Kwa kuwa, Mdhamini wetu mkuu SportPesa anazuiwa kikanuni kwenye mashindano ya CAF, mkataba kati ya Yanga na SportPesa hauizuii Klabu ya Yanga kutafuta Mdhamini mbadala kwenye nafasi hiyo, hivyo basi Klabu ikaamua kuingia makubaliano ya udhamini na Kampuni ya Haier kwa ajili ya mashindano ya CAF pekee. Kwa maelezo hayo, Klabu inathibitisha kuwa haijavunja kipengele chochote cha mkataba wake na SportPesa.

Mnamo saa 1:52 usiku wa tarehe 30 Januari, 2023, siku ya uzinduzi wa jezi maalumu kwa ajili ya michuano ya CAF zenye nembo ya Mdhamini Haier, Klabu ilipokea barua pepe kutoka kwa Mdhamini wetu mkuu SportPesa, wakiielekeza klabu kutumia nembo ya “Visit Tanzania” kwenye nafasi ya mbele ya jezi kwa ajili ya mashindano ya CAF na ikiishinikiza klabu kuhudhuria uzinduzi wa jezi hizo siku inayofuatia, tarehe 31, Januari 2023, saa 5:00 asubuhi kwenye ofisi zao.

Klabu ya Yanga ilitafsiri maamuzi haya ya SportPesa ni kitendo kisicho na mantiki na chenye dhamira ovu na kinachokiuka makubaliano ya kimkataba kwa pande zote mbili.

Klabu ya Yanga inatambua kwamba, nembo ya “Visit Tanzania” sio chapa wala mpango wa Mdhamini wetu SportPesa, hivyo tusingeweza kutumia nembo hiyo bila maridhiano na mmliki wa nembo hiyo.

Klabu inapenda kuujulisha umma kuwa, hatujatafutwa na taasisi yoyote kuhusiana na matumizi ya nembo ya “Visit Tanzania” hivyo hatukukataa kutumia nembo hii kama ilivyoelezwa na SportPesa.

Tunapenda pia kuukumbusha umma kuwa, Klabu yetu ilishawahi kutumia nembo ya “Visit Zanzibar and Kilimanjaro” kwa ajili ya kuitangaza nchi yetu kwenye mashindano ya CAF msimu uliopita hivyo basi, hatuna dhamira ya kukataa kuitumia nembo ya “Visit Tanzania” msimu huu.

Tamko la SportPesa kuwa Klabu ya Yanga imekataa kutumia nembo ya “Visit Tanzania”  lina taswira ya kuonyesha kuwa Klabu ya Yanga imekosa uzalendo na lina nia ya kuigombanisha klabu ya Yanga na Serikali pamoja na Wananchi wake. Klabu ya Yanga inasisitiza kuwa, hatukubaliani na kashfa ya aina hii kwa namna yoyote ile.

Uongozi wa Yanga unaendelea kusisitiza kuwa haujakiuka makubaliano yoyote ya kimkataba kati yetu na SportPesa na hauna nia ya kufanya hivyo. Mkataba hauizuii klabu kutumia nembo ya Mdhamini mwingine inapotokea mazingira yanayoizuia kutumia nembo ya Mdhamini mkuu.

Hivyo basi, uongozi wa klabu ya Yanga, unautaarifu umma kuwa jezi zetu zenye nembo ya Haier, zitatumika kwenye mechi za michuano ya Kombe la Shirikisho la CAF pekee.