1: Yanga imesajili Mamadou Doumbia baada ya kununua mkataba wake kutoka timu ya Stade Malien ya Mali. Sio usajili wa bure au mkopo.

2: Kwa mara nyingine tena, Yanga imeonyesha msuli wa kiuchumi kwenye soko la usajili na nguvu kubwa ya ushawishi kutoka kwa Rais Eng. Hersi Said. Kwa kifupi, Rais wa Yanga, Hersi amethibitisha yeye ni ‘Pele wa Usajili’ barani Afrika.

3: Doumbia ni beki tegemeo wa timu ya Stade Malien na nahodha wa timu ya taifa ya Mali inayoshiriki mashindano ya CHAN inayoendelea kule Algeria. Ni kwanini usajili huu ni mkubwa sana kwa Yanga na Ligi ya Tanzania kwa ujumla?

4: Kitendo cha Doumbia kusaini Yanga, tafsiri yake ameichagua jezi ya Wananchi na sio mashindano ya CHAN. Yaani Mamadou amevutiwa zaidi na Project ya Yanga ambayo ina mengi mazuri ya kumuendeleza kama mchezaji.

5: Ni usajili mkubwa kwa Ligi ya Tanzania pia. Huyu ni nahodha wa timu ya taifa ya Mali ya ndani. Usajili huu umeishtua sana Afrika na umefanya wengi kuona thamani na ukubwa wa Ligi yetu kupitia usajili wa Doumbia.

6: Nini Doumbia anakwenda kukiongeza Yanga? Kwanza ni uzoefu. Mamadou alikuwepo kwenye kikosi cha Mali kilichocheza CHAN 2021. Mashindano ambayo Mali walikwenda hadi hatua ya Fainali.

7: Uzoefu wa wachezaji wengi wa kimataifa kuanzia Diarra, Doumbia, Bangala, Djuma, Mayele, Aziz KI na wengine unawapa Yanga nguvu kiufundi kwenye mashindano ya CAF msimu huu. Wanaweza kuota makubwa zaidi.

8: Doumbia hatakuwa mchezaji mgeni Yanga. Tayari atamkuta Diarra, kipa aliyewahi kucheza nae kabla kwenye mashindano tofauti tofauti. Kiufundi, hapa Yanga wamefanya usajili mkubwa na kwa umakini sana.

9: Msimu huu Yanga wameruhusu mabao 10 kwenye Ligi Kuu, asilimia kubwa ni mabao yaliopatikana kwa mashambulizi ya mipira ya juu. Ubora wa Doumbia kwenye ‘Aerial Balls’ utakuja kutibu tatizo hili.

10: Yanga imeongeza upana na ubora wa kikosi chao unaokwenda kumpa ‘option’ nyingi Profesa Nabi kwenye mbinu zake.