WANANCHI tumeondoka kwenye Kombe la Mapinduzi kibabe kwa ya kuvuna pointi 4 kwenye Kundi B, baada ya sare ya bao 1-1 dhidi ya Singida Big Stars.

Matokeo hayo yameifanya Singida Big Stars kufuzu hatua ya nusu fainali kwa faida ya mabao ya kufunga na kufungwa, licha ya kulingana pointi na Yanga kwenye kundi hilo.

Singida wana tofauti ya mabao mawili baada ya kuifunga KMKM 2-0 kwenye mchezo wa kwanza huku Yanga wakiwa na tofauti ya bao 1 baada ya kuifunga KMKM bao 1-0.

Bao pekee ya Yanga kwenye mchezo wa leo dhidi ya Singida Big Stars lilifungwa na David Bryson kwa mkwaju mkali wa mpira uliokufa dakika 30 ya mchezo.

Kiungo mpya wa Yanga, Mudathir Yahya alibeba tuzo ya mchezaji mwenye nidhamu kutoka kwa jopo la makocha waliompigia kura.

Akizungumza na YANGA MEDIA baada ya tuzo hiyo, alisema amefurahi kuvaa jezi ya Yanga na anaamini michuano hii ya Mapinduzi itamjenga kuwa bora zaidi Ligi Kuu ya NBC msimu huu.

“Namshukuru Mungu nimecheza salama na nimeiwakilisha klabu yangu kwenye mashindano haya, naamini imenisaidia na itanipa nguvu kuelekea Ligi Kuu na mashindano ya kimataifa,” alisema Mudathir.