UONGOZI wa Yanga chini ya Rais Eng Hersi Said, Benchi la ufundi na wachezaji leo wamemtembelea Mama Fatma Karume pamoja na wajumbe wa Bodi ya Wadhamini na kuwakabidhi makombe manne tuliyoshinda msimu uliopita.

Hafla hii iliyofanyika nyumbani kwa Mama Fatma Karume, maeneo ya Maisara, Zanzibar imekuwa ni mara ya kwanza kwa Uongozi wa Yanga kukutana na Bodi ya Wadhamini tangu timu hiyo ilipobeba makombe hayo mwaka jana.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mama Fatma Karume alionyesha furaha yake na kuwapongeza wachezaji kwa mafanikio hayo ya kubeba mataji manne ya mashindano ya ndani.

“Nimefurahi sana na ninawapongeza sana wachezaji wetu kwa kupambana kwa nia moja kuhakikisha Yanga inabeba makombe yote haya manne, hii ni heshima kubwa kwa klabu yetu yenye historia kubwa Afrika nzima,” alisema Mama Karume.

Pia Mama Fatma Karume alitoa nasaha kwa wachezaji akiwaomba wapambane zaidi kwa ajili ya kufanya vizuri zaidi na kwenye michuano ya kimataifa.