ZOEZI la usajili wa kidijitali linaendelea hapa Zanzibar, ambapo timu nzima ya Kilinet na Yanga wapo kwa ajili ya kuwasajili kidijitali kuwa Wanachama au Shabiki, na kutoa elimu kuhusiana na uanachama.

Zoezi hili litaendelea kufanyika  hapa kwa siku nne ikiwa ilianza jana maeneo ya Uwanja wa Amaan na leo  kuendelea hapa maeneo ya Kariakoo, lakini zoezi hili litaendelea na kutamatika siku ya Jumamosi.

Afisa Muhamasishaji wa Yanga, Priva Shayo alisema huu ndio wakati wa viongozi wa matawi kuchangamkia fursa na kuwahimiza Wanachama wao kujisajili kidijitali,

Kimsingi ujio wetu Zanzibar umekuwa faraja kwa mashabiki wetu ambao kwa muda mrefu walikuwa na matamanio ya kupata kadi zao. Tunafahamu bado kuna kiu kubwa kwa wenyeji wa visiwani kupata kadi zao na tunafahamu kuna kundi kubwa sana la wanachama wetu ambao wana matamanio makubwa ya kujisajili.  Kiujumla hatujawafikia kwa ukubwa ambao tumejipanga nao. Hata hivyo Tunazidi kusisitiza viongozi wa matawi kutimiza majukumu yao ya kikatiba na kusajili wanachama wengi kwa kadiri ya uwezo wao. Kesho tunaendelea na zoezi hili katika uwanja wa Amani na tutaangalia uwezekano wa kwenda maeneo mengine kadiri ya muda na ratiba ya timu yetu hapa visiwani.”

Naye Katibu wa Tawi la Kiembe Samaki hapa Mjini Magharibi; Emmanuel Gema Magulu alisema:
“Zoezi hili lina umuhimu sana kwetu kama wanayanga hapa Zanzibar, kumekuwa na muamko mkubwa huku Visiwani wa kujisajili kidijitali. Ombi langu ni klabu ifikirie kuongeza muda wa kuendesha zoezi hili hapa ili kuwafikia wananchi wengi hata waliopo huko shamba na nje ya mji kidogo”

Nassor Chombo,mwanachama na katibu wa Tawi la Kijangwani alishukuru kwa zoezi hili kufika visiwani hapa na kusema walikuwa wakisubiri kwa hamu kubwa,

“Tuliwasubiri sana hapa Zanzibar, maana kuna Wananchi wengi sana wanaohitaji hizi kadi na wengine walijisajili ila hawakupata kadi zao. Sasa kwa zoezi hili la kujisajili na kupata kadi yako papo hapo imeamsha ari ya kujisajili kwa kasi zaidi”

Zoezi hili litaendelea tena hapo kesho kwenye Uwanja Wa Amaan.