BAADA ya ushindi wa bao 1-0 tulioupata dhidi ya KMKM jana, kikosi chetu kinakabiliwa na mchezo mwingine wa Kundi B dhidi ya Singida Big Stars siku ya kesho.

Mchezo huo utakaopigwa majira ya saa 2:15 usiku ndio utakaoamua nani anafuzu kutoka kwenye kundi baada ya wawili hao kulingana pointi mpaka sasa.

Mchezo wa kwanza Singida Big Stars walishinda bao 2-0 dhidi ya KMKM hivyo wao kuwa kwenye nafasi ya kuhitaji sare tu waweze kusonga mbele.

Kutambua umuhimu wa hilo, kocha Cedric Kaze leo atakuwa na ratiba ya mazoezi na kikosi cha Yanga kuanzia saa 11:00 jioni kwenye uwanja wa Mao.

Akizungumza na YANGA MEDIA kocha Kaze amesema mchezo wa mwisho utakuwa mgumu sana kutokana na ubora wa kikosi cha Singida Big Stars lakini kama vijana wake watakuwa makini na kucheza kwa kujiamini basi bila shaka nafasi ya kufanya vizuri bado ipo.

“Tuliwaona Singida kwenye mechi ya kwanza, ni timu nzuri na wamekuja kwenye mashindano haya na kikosi chao kamili.

“Naamini utakuwa mchezo mzuri sana kwani wachezaji wameonyesha kujiamini na kuwa tayari na mchezo huo. Ni imani yangu mazoezi ya leo yatatupa maandalizi mazuri kuelekea mchezo huo,” alisema Kaze.