KIUNGO Mudathir Yahya amesema kiungo wa zamani wa Yanga, Abdi Kassim ‘Ballack wa Unguja’ ni miongoni mwa nyota waliomvutia kujiunga na kikosi cha Wananchi.

Mudathir ameripoti kwa mara ya kwanza kambini na kufanya mazoezi ya mwisho na wachezaji wenzake kuelekea mchezo wa kwanza wa Kombe la Mapinduzi dhidi ya KMKM.

Akizungumza na YANGA MEDIA, Mudathir amesema nyota wengi kutoka Zanzibar wamepita Yanga lakini kwake aliyemvutia zaidi hadi na yeye kutamani kuvaa jezi ya Wananchi.

“Wachezaji wengi wa Zanzibar wamepita hapa lakini kwangu ukiniuliza ni yupi amekutuvia zaidi nitakutajia Abdi Kassim.

“Alikuwa kiungo mwenye ufundi, nidhamu na mpambanaji. Vijana wengi wa Zanzibar tulivutiwa na uchezaji wake na kutamani siku moja na sisi tuvae jezi ya Yanga,” alisema Mudathir.