GOLIKIPA bora wa Ligi Kuu ya NBC msimu uliopita, Djigui Diarra bado yupo sana kwa Wananchi.

Hii inakuja baada ya golikipa huyu raia wa Mali kuongeza mkataba wa kubakia Yanga mpaka msimu wa 2024/25.

Diarra alijiunga na Yanga mwanzoni mwa msimu wa 2021/22 akitokea katika klabu ya Stade Malien ya Mali.

Akizungumza na YANGA MEDIA, Diarra amesema ni furaha kubwa kwake kuongeza mkataba ndani ya klabu ya Yanga na kuahidi kuendelea kuipambania Yanga kutwaa mataji mengi zaidi.

Ni siku ya furaha sana kwangu, nashukuru kwa Uongozi wa Yanga kwa kuniongeza mkataba. Yanga ni klabu kubwa Afrika na bila shaka ni ndoto ya wachezaji wengi kucheza hapa.

“Niwaahidi mashabiki wa Yanga kuwa nitaendelea kujituma na kuhakikisha timu yetu inafanya vyema kwenye michuano ya ndani na Kimataifa,” alisema Diarra.

Naye Rais wa Yanga, Eng Hersi Said amewaahidi wanachama na mashabiki wa Yanga kuwa uongozi unaendelea na mazungumzo ya kuongeza mikataba ya baadhi ya wachezaji wanaomaliza mikataba kama ilivyopendekezwa na benchi la ufundi.

“Tunaendelea kufanyia kazi ripoti ya benchi la ufundi, sisi kwa sasa hatujengi timu, hiyo hatua tulishaivuka misimu kadhaa nyuma. Sasa hivi tunaendelea na mazungumzo na wachezaji wetu nyota kuhakikisha wanabaki na kuendelea kuwapa furaha mashabiki wetu.

“Diarra ni mmoja wa wachezaji muhimu kwenye kikosi chetu, kama uongozi tuna furaha amekubali kubaki kuendelea kuvaa jezi ya Yanga,” alisema Hersi.