Rais wa Yanga, Eng. Hersi Said anapenda kutoa salamu za kuaga Mwaka 2022 na kuukaribisha Mwaka 2023 kwa Wanachama na Mashabiki wa Klabu ya Yanga.

Mwaka 2022 ulikuwa wenye mafanikio mengi kwa Klabu yetu, ikiwemo kutwaa mataji matatu ndani ya msimu wa 2021/ 2022.

Mataji tuliyotwaa ni Ngao ya Jamii, Ligi Kuu ya NBC na Kombe la Shirikisho la Azam.

Lakini pia Klabu yetu ya Yanga imeweza kubeba ubingwa mwingine wa Ngao ya Jamii, ikiwa ni ufunguzi wa msimu wa 2022/23.

Mafanikio mengine makubwa kwa Klabu yetu ya Yanga ndani ya Mwaka 2022 ni kuweka rekodi ya kucheza mechi 49 za Ligi Kuu bila kupoteza.

Rekodi hii ni ya kwanza kwenye historia ya soka la Tanzania lakini pia ni ya nne kwenye rekodi kwa Afrika kwa timu zilizocheza mechi nyingi za Ligi bila kupoteza.

Tunajivunia pia mwaka 2022 kwa Klabu yetu ya Yanga kufanya vyema kwenye michuano ya kimataifa kwa kuweza kufuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho la CAF.

Kwa kipekee kabisa, Eng. Hersi anapenda kutoa shukrani zake za dhati kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mazingira mazuri kwenye sekta ya michezo kwa mwaka 2022.

Eng. Hersi pia anatoa shukrani kwa Wizara ya Michezo, Sanaa na Utamaduni, Shirikisho la Soka TFF, Bodi ya Ligi na wadau mbalimbali wa mchezo wa mpira wa miguu nchini kwa mengi mazuri waliyoyafanya kwa kushirikiana na Klabu yetu.

Ndugu, Wanachama na Mashabiki wa Klabu ya Yanga, umoja, mshikamano na upendo ndio ilikuwa siri kubwa ya mafanikio yetu ya Mwaka 2022.

Hivyo basi, wakati huu tukiuanza mwaka 2023 tukiwa vinara wa Ligi Kuu ya NBC, ni jukumu letu sote kuendelea kuiunga mkono timu yetu ili tuweze kufikia malengo yetu tuliyonayo kwa mwaka huu mpya, ikiwemo kutetea mataji yetu ya mashindano ya ndani na kufanya vizuri zaidi kwenye michuano ya Kimataifa.

Mungu ibariki Young Africans Sports Club.

Daima mbele nyuma mwiko.

Eng. Hersi Said
Rais Young Africans SC