Kocha msaidizi wa Yanga SC Cedric Kaze amesema kuwa mchezo ujao dhidi ya Simba SC ni mchezo muhimu sana kwa klabu kurejesha hali yake ya kujiamini kwa kila mmoja.

Kaze amesema mchezo uliopita dhidi ya Al Hilal ulivuruga mipango yetu lakini bado tuna matumaini ya kufanya vizuri.

Kaze ana maoni gani kuhusiana na mchezo uliopita?

“Mradi wetu umeandaliwa tokea msimu uliopita ambapo tulibeba mataji kadhaa. Tumeondolewa ligi ya mabingwa lakini huu sio muda wa kujilaumu sana isipokuwa kuheshimu wapinzani na kusonga mbele kukabiliana na changamoto zinazotuhusu kwa sasa.”

Nini maoni yake kwa mchezo ujao?

“Mchezo ujao ni muhimu mno kwa sababu najua ushindi utarejesha tena ile morali tuliyokuwa nayo. Malengo yetu hayajafa yamepungua tu kwa kiasi fulani. Simba ni timu kubwa na hii ni Derby hivyo tunawaheshimu sana Simba SC na tumejipanga vyema kukabiliana nao”

Mechi ngumu kama hizi zinampa changamoto kwa kiasi gani?

“Sisi kama viongozi wa benchi la ufundi huwa tunapenda sana kusimamia michezo mikubwa yenye presha kubwa kwa sababu ni mechi ambazo zinakupa majibu sahihi ya kile ulichojiandaa nacho. Ni aina ya mechi ambazo zinakupa mwanga sahihi maendeleo ya mbinu zako”

Amewahi kuitumika Yanga kwenye Derby kadhaa je anacho kitu cha ziada kwa sasa?

“Kinachotupa matumaini kwa sasa ni aina ya wachezaji tulio nao. Tuna wachezaji wazuri sana wenye uwezo wa kuhimili presha za mechi kubwa kama hizi vile vile wachezaji ambao wanaweza kuhimili presha hasa katika kipindi kama hiki ambacho Tunajua matokeo yaliyopita yametufadhaisha” Alisema Kaze.