Timu ikiwa inajiandaa na mechi yake ya kwanza ya ligi ya mabingwa Afrika, leo wachezaji wamefanya mazoezi ya mwisho kuelekea mchezo huo dhidi ya mabingwa wa Sudan ya Kusini, Zalan FC.

Tumepata wasaa wa kuongea na kocha msaidizi; Cedric Kaze ambae ameongelea mambo kadhaa kuhusu mchezo huo.

Kuhusu Majeruhi:

“Tuna majeruhi ambao walitokea kwenye game ya Azam, Bernard Morrsion ameumia na Sureboy pia alikuwa na majeruhi ambayo unaweza sema yameongezeka baada ya kuingia kwenye ule mchezo kwa hiyo hawa kesho hawataweza kutumika.

“Dickson Job bado yupo kwenye uangalizi, ila jana amefanya mazoezi vizuri, na leo pia hivyo tunahisi anaweza kutusaidia kwenye mchezo wetu hio kesho. Lazarous Kambole pia tunaangalia namna gani anaweza kutusaidia”

 

Kuhusiana na Zalan FC:

“Kitu kibaya ni kwamba hatuna taarifa za uhakika za kutosha kuhusiana na wapinzani wetu, lakini tutatumia dakika za mwanzo za mchezo kujua wanachezaje.”

“Ni kitu ambacho tumeongea kuanzia Jumatano, kuwa hatuwezi kudharau timu hata moja. Timu ambayo imefika Ligi ya Mabingwa Afrika sio timu ndogo. Soka nchini Sudan Ya Kusini imebadilika, kwa sababu nchi yao imeendelea na sio Sudan ya Kusini ile tulioijua miaka 10 iliopita.”

“Hivyo tunajua tunaenda kucheza na bingwa wa nchini kwao na tutacheza kwa tahadhari zote tukirekebisha makosa yote yaliojitokeza kwenye mchezo dhidi ya Azam FC na tukiwa tunazingatia kilichotokea mwaka jana kisitokee mwaka huu.”

Kuhusu maandalizi ya timu:

“Maandalizi ni mazuri japo hayakuwa marefu kwa kuwa tulikuwa na mechi nyingine ya ligi kuu dhidi ya Azam siku ya Jumanne na kesho tuna mechi nyingine ya Ligi ya Mabingwa,ila kwa ujumla timu ipo tayari kaikili na kiafya”.