Baada ya sare ya goli 2-2 dhidi ya Azam FC siku ya Jumanne, Yanga wameanza kujiandaa na mchezo wa kimataifa dhidi ya Zalan FC ya Sudan Kusini,ikiwa ni mechi ya kwanza kweye hatua ya awali kutafuta tiketi ya kufuzu kwenda kwenye hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Zalan FC ambao ndio mabingwa wapya wa Ligi ya Sudan Kusini (South Sudan National League) mwaka 2022 ni wenyeji wa mji wa Rumbek uliopo kilomita 300 nje ya mji mkuu, Juba; na  wanatumia uwanja wa Rumbek Freedom Square kwa ajili ya mechi zao za ligi.

Japokuwa sio wakongwe sana kwenye soka nchini humo, Zalan FC walifanikiwa kupata Mafanikio ya haraka haraka ikiwepo kuchukua ubingwa wa ligi kuu msimu uliopita, lakini waliwahi kuchukua ubingwa wa Sudan League Cup mwaka 2018.

Zalan FC -Mabingwa wa Sudan Kusini 2022.

Yanga ambao ni mabingwa wa kihistoria hapa nchini watakuwa wanashiriki mashindano haya wakiwa na kumbukumbu mbaya ya kutolewa hatua ya awali msimu wa 2021/22 dhidi ya Rivers Utd ya Nigeria.

Wakiwa katika viwango bora kabisa kwa muda mrefu, Yanga atavaana na Zalan Fc wakiwa wanaendeleza rekodi yao ya kutokufungwa tangu msimu uliopita.

Hatua hii ya awali itashuhudia Yanga wakicheza michezo miwili dhidi ya Zalan Fc, nyumbani na ugenini lakini kutokana na uwanja wa Rumbek Freedom Square kutokidhi vigezo vya CAF, watatumia uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar Es Salaam siku ya Jumamosi ya tarehe 10 Septemba saa 10:00 jioni.

Young Africans SC