Young Africans SC usiku huu wamecheza mechi yao ya kwanza nyumbani kwenye dimba la Benjamin Mkapa Stadium na kutoka sare ya magoli 2-2 dhidi ya Azam katika mchezo wa Ligi Kuu NBC (NBCPL).

Mchezo huo uliokuwa wa kasi huku timu zote mbili zikionesha soka safi lililovutia, Azam Fc walikuwa wa kwanza kupata goli kupitia beki wao, Daniel Amoah mnamo dakika ya 23 baada ya kuunganisha mpira wa adhabu uliopigwa na Ayub Lyanga

Azam FC ilikuwa imara kuzuia kila shambulizi la Yanga kwa kipindi chote cha kwanza, na kufanya kwenda mapumziko wakiwa wanaongoza kwa goli 1.

 

Lomalisa Mutambala

Kipindi cha pili kilianza kwa mwalimu Nasrdeen Nabi kufanya mabadiliko kidogo kwa kumtoa Dennis Nkane na nafasi yake kuchukuliwa na Feisal Salum ‘Fei Toto’ huku Dickson Job aliepata majeraha kipindi cha kwanza alimpisha Djuma Shaaban.

Dakika ya 56 , krosi ya Bernard Morrison iliokolewa na mpira huo uliokuwa ukizagaa nje ya eneo la hatari ulikutana na Feisal aliepiga shuti kali lililomshinda kipa wa Azam Fc.

 Katika mechi iliokuwa imejaa ufundi na mbinu nyingi, Azam Fc walipata bao la pili dakika ya 64 baada ya Malickou Ndoye kumalizia mpira uliopigwa na Abdul Selemani ‘Sopu’.

Muda mchache baadae, Morrison alifanyiwa madhambi ndani ya box na refa kuwapa Yanga penati, ambayo Djuma Shaaban alikosa.

Yanga waliendelea kucheza kwa kasi na kutawala mpira kwa muda mwingi ambapo dakika ya 76, Khalid Aucho alimtengea mpira Feisal Salum ambae kwa mguu wake wa kulia alipiga shuti kali ambalo nalo lilimshinda kipa wa Azam Fc Ally Ahamada na kufanya mchezo kuwa 2-2.

Fiston Mayele

Baada ya mchezo huu, Yanga watarudi mazoezini kujiandaa na mchezo wa kwanza wa kimataifa kutafuta tiketi ya kufuzu kwenda hatua ya makundi ya Ligi Ya Mabingwa Afrika, wakicheza dhidi ya Zalan Fc ya Sudan ya Kusini siku ya Jumamosi, September 10 ndani ya dimba la Chamazi Complex – Dar Es Salaam.

Kikosi Kilichoanza: Diarra,Job,Lomalisa,Mwamnyeto (C), Bangala, Aucho, Bigirimana, Morrison, Mayele, Ki Aziz, Nkane.

Subs: Mshery,Bacca,Djuma,Feisal,Sureboy,Mauya,Ambundo,Makambo,Clement.