Yanga pamoja na GSM wametambulisha jezi mpya zitakazotumiwa na mabingwa wa NBC Premier League kwa msimu wa 2022/23.
Jezi hizo zilizobuniwa na mbunifu wa mavazi nchini, Sheria Ngowi zimebeba maudhui mbali mbali yenye kuelezea uzuri wa taifa letu pamoja na kuelezea historia na tunapoelekea kama klabu.
“Hadithi yetu ya jezi ya nyumbani imeanzia kwenye kutangaza maeneo yote muhimu na ya kihistoria kwenye nchi yetu kama Mlima Kilimanjaro, Nyerere Square Dodoma, Ngome Kongwe Zanzibar na kadhalika” – alisema mbunifu Sheria Ngowi.
Huku jezi ya ugenini inaelezea muunganiko wa matawi ya Wanachama wa Yanga Tanzania nzima ikichagizwa na mfumo wa mabadiliko (transformation).
“Hadithi yetu ya jezi ya Tatu inawahusisha Wachezaji wetu wa zamani (legends) kwa kufanya makubwa katika sehemu ya historia ya Klabu yetu na jezi hii imebuniwa kwa kuwaandika majina yao kwa mfumo wa sahihi” – Sheria aliongezea.
Hafla ya kuzindua jezi hizo ilifanyikia kwenye ukumbi wa kimataifa wa Serena Hotel, Dar Es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi wa ngazi za juu klabuni, wakiongozwa na Rais, Eng. Hersi Said, Makamu wake Arafat Haji, mtendaji mkuu wa klabu – Senzo Mbatha, wajumbe wa kamati tendaji na Abbas Tarimba mkurugenzi wa wadhamini wetu wakuu, Sportpesa.
“Niendelee kuunga mkono jitihada mbalimbali ambazo kampuni ya GSM inaendelea kuzifanya, kwa kuongeza thamani ya jezi zetu ambapo itaenda kuongeza mapato ya Young Africans SC, ambapo mapato hayo yanaenda kuisaidia klabu kuendesha shughuli zake” alisema Rais wa klabu, Eng. Hersi Said.
Kwa upande wa mtendaji mkuu wa klabu Senzo Mbatha alisema “Tupeleke shukrani kwa Sheria Ngowi na kazi nzuri aliofanya kwa kuandaa dhana mbali mbali zinazoelezea historia ya klabu na nchi. Ili kujenga klabu bora inapaswa kujiandaa kupata matokeo uwanjani na kuwa wabunifu katika matukio kama haya ya ubunifu wa jezi ambayo ni chanzo cha mapato ya klabu.”
Jezi hizo zimeanza kupatikana nchini kote kwa bei ya shilingi 35,000.