JIONI ya leo, kikosi cha timu yetu ya Young Africans SC, kimecheza mechi ya kirafiki kujiweka sawa kuelekea mchezo ujao wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Vital’O.
Mchezo huo wa kirafiki uliochezwa kwenye uwanja wetu wa mazoezi uliopo Avic Town, Kigamboni, Young Africans imeibuka na ushindi wa magoli 4-0 dhidi ya Green Warrirs.
Wafungaji wa magoli hayo ambayo yote yamefungwa kipindi cha kwanza ni Kennedy Musonda, Clatous Chama, Jean Baleke na Duke Abuya.
Kucheza mechi hiyo ya kirafiki ni sehemu ya kukiweka sawa kikosi kilichotoka kushinda Ngao ya Jamii, huku pia Jumamosi ijayo ya Agosti 17, 2024 tukiwa na mechi dhidi ya Vital’O ya Burundi katika mchezo wa kwanza hatua ya awali wa Ligi ya Mabingwa Afrika.
Baada ya mchezo huo wa kwanza, tutarudiana Agosti 24, 2024 huku yote ikichezwa Dar es Salaam kutokana na wapinzani wetu kuuchagua Uwanja wa Azam Complex kwa mechi zao za nyumbani baada ya kukosa viwanja vyenye hadhi ya kimataifa nchini kwao Burundi.