RAIS wa Klabu ya Young Africans SC, Injinia Hersi Said, amewapongeza wachezaji na benchi la ufundi kwa namna timu inavyocheza soka la kuvutia na kupata matokeo mazuri huku akisema timu sasa ipo levo nyingine kabisa.
Hersi ambaye amekuwa akifanya kazi kubwa sana ya kujenga timu kwa kusajili wachezaji wenye viwango vikubwa na kuwabakisha wale wanaohitajika ndani ya timu licha ya kutakiwa na vigogo wa soka Afrika, amesema anajivunia kuona timu imefika levo ya juu kiuchezaji.
Akizungumza baada ya kubeba Ngao ya Jamii kwa kuifunga Azam magoli 4-1, Hersi amesema: “Nilikuwa ninautazama mchezo kwa heshima na taadhima, ulikuwa mzuri, Azam walionesha kiwango kizuri ilikuwa kweli ni fainali lakini sisi Young Africans tumeonesha levo ambayo tupo, ni levo nyingine kabisa.
“Nichukue fursa hii kuwapongeza benchi la ufundi lakini pia mashabiki na wapenzi wa klabu hii kwani siku zote wao wamekuwa nyuma ya kufanya sisi tutafute vilivyo vizuri zaidi.
“Wapo watu ambao walikuwa wanataka kuiona Young Africans katika ubora huu na huo ubora leo umeonekana.
“Licha ya kuwa chini kwa goli moja hakikuwa kitu ambacho kimeturudisha nyuma kama timu, tulitafuta matokeo tukayapata na baadaye tukacheza kwa nidhamu. Niwapongeze wachezaji na benchi la ufundi.
“Wakati tunaingia katika uongozi tulisema tunataka kuijenga hii timu kuwa imara, huu ndio uimara tuliokuwa tunauzungumza. Na hii bado, safari haijafika mwisho, tutaendelea kuboresha kila siku.
“Unaweza kuona tumemuongeza mchezaji kama Chadrack Boka, watu walikuwa hawaelewi vipi anakuja mchezaji wakati tunaye bora kama Lomalisa, bila ya kumvunjia heshima Lomalisa ni kweli alikuwa mchezaji mzuri na ametoa mchango mkubwa kwenye timu yetu lakini timu inatakiwa kujengwa kila msimu kwa kuleta wachezaji wenye ubora zaidi waje kukusaidia kutoka pale ulipokuwa kwenda levo ya juu zaidi.
“Mechi ya fainali kushinda goli nne sio kitu cha mzaha na baadhi ya nafasi hatujazitumia vizuri yangeweza kuwa madhara makubwa zaidi.”