BAADA ya kuwa washindi wa Kombe la Toyota, kikosi cha timu yetu ya Young Africans kinatarajia kuwasili Dar es Salaam saa 9 alfajiri kikitokea Afrika Kusini.
Jana Jumapili, Young Africans tulishinda magoli 4-0 dhidi ya Kaizer Chiefs na kubeba kombe hilo. Wafungaji wa magoli hayo ni Stephane Aziz Ki aliyeweka kimiani mawili, Prince Dube na Clement Mzize.
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Young Africans, Ally Kamwe, amewataka mashabiki na wanachama kujitokeza Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam kuwapokea mashujaa wetu.
Kamwe amesema itapendeza kuanzia saa 5 usiku leo kufika uwanjani hapo kabla ya kikosi kutua saa 9 alfajiri, kisha zoezi la kuwalaki mashujaa wetu litaanza.
Aliongeza kwamba, baada ya kikosi kuwasili, wachezaji watapewa nafasi ya kwenda kupumzika kisha mashabiki na wanachama watafanya paredi kushangilia ubingwa huo hadi Makao Makuu ya Klabu yaliyopo Jangwani.
“Siku ya leo tuna mapokezi makubwa, Yanga ni mabingwa wa kombe jipya la Toyota Cup tuliloshinda huko Afrika Kusini, Timu itawasili saa tisa usiku, niwaombe mashabiki na wanachama tujitokeze kwa wingi kuwapokea wanajeshi wetu.
“Twendeni leo pale Airport tuwaoneshe tunaanza kwa kishindo msimu huu, niliwaambia kuanzia saa tano usiku tumekamilika wenye ngoma, matarumbeta na watu wote kwenye matawi wajitokeze kazi yetu kucheza, kula na kusubiri timu yetu iwasili.
“Wakiwasili saa tisa, wachezaji watapokelewa na kuwaacha wakapumzike, ila sisi tutaendelea na parade ya kuleta kombe hapa makao makuu,” alisema Kamwe.