Meneja wa Young Africans SC, Walter Harson, amezungumzia hali ya kikosi baada ya kusafiri kutoka Dar es Salaam alfajiri ya jana na kufika mchana wake nchini Afrika Kusini.
Young Africa SC ipo Afrika Kusini kwa ajili ya mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Mamelodi Sundowns baada ya ule wa kwanza uliochezwa Dar es Salaam kumalizika kwa matokeo ya 0-0.
Harson ameanza kuzungumzia safari ilivyokuwa kutoka Dar es Salaam hadi Pretoria, Afrika Kusini na namna kikosi kilivyopokelewa, kisha kufanya mazoezi ya kwanza.
“Safari ya kikosi cha Young Africans kutoka Dar es Salaam kuja hapa Afrika Kusini kwenye Mji wa Pretoria imeweza kwenda vizuri kupitia pale nchini Malawi na hatimaye kikosi kimefika katika Mji huu wa Pretoriana kupokelewa vizuri sana na Ubalozi wa Tanzania hapa nchini Afrika Kusini.
“Baada ya mapokezi pale kwenye Mji wa Johannesburg, kikosi kimekuja moja kwa moja kwenye Mji wa Pretoria ambapo mchezo utaweza kuchezwa siku ya Ijumaa majira ya saa 2 usiku kwa saa za hapa Afrika Kusini, lakini saa 3 ya usiku kwa saa za nchini Tanzania.
“Kila kitu kimeenda vizuri kwa siku hii ya leo (jana Jumanne) na kama unavyoona siku ya kwanza kikosi kikiwa kinafanya mazoezi baada ya safari ndefu kujiweka vizuri.
“Program zitaendelea kwa siku ya kesho (leo Jumatano) kufanya mazoezi kwa siku ya pili kabla ya siku ya Alhamisi kwenda kufanya mazoezi ya mwisho kwenye uwanja ambao tutaucheza mchezo huo kwenye majira ya saa 3 kwa saa za Tanzania.
“Kila kitu kinaenda vizuri mpaka sasa hivi, Wananchi popote pale mlipo tunajua sapoti yenu ni kubwa sana kwa timu yenu, mashabiki wetu ambao wapo njiani kutoka nchini Tanzania kuja kutua sapoti, mashabiki ambao wanatoka nchi Jirani tunawahitaji kwa kiasi kikubwa sana kuweza kutupa nguvu kuelekea kwenye mchezo huu wa tarehe 5, mchezo ambao tuna imani kabisa tunakwenda kuandika historia.
“Kila kitu kinaendelea sawa mpaka sasa hivi hapa Afrika Kusini na tunaamini lengo ambalo tumedhamiria kulifanya la kwenda hatua inayofuata ya nusu fainali kwa mara ya kwanza tunaenda kuandika historia hiyo siku ya Ijumaa.
“Wananchi endelea kutupa sapoti, kwa wale ambao wapo nyumbani endeleeni kutuombea dua, tunaamini kabisa tunaenda kufanya jambo ambalo linaenda kuishtua Afrika. Wananchi kuweni tayari mambo mazuri yanakuja,” alisema Harson.