NADIR Haroub. Kutokana na ubora wake uwanjani mashabiki wakampachika jina la Cannavaro. Wakimfananisha na beki wa zamani wa Italia, Fabio Cannavaro.

Ni gwiji wa klabu yetu. Kwenye miaka 12 aliyocheza Yanga SC baada ya kujiunga nayo mwaka 2006 akitokea Malindi ya Zanzibar ameshinda jumla ya mataji 18 yanayomfanya awe mchezaji mwenye mafanikio makubwa kuliko mwingine kwenye kikosi cha Yanga kuanzia mwaka 2000 hadi sasa.

Cannavaro ameshinda mataji saba ya Ligi Kuu Tanzania Bara mwaka 2006, 2008, 2009, 2011, 2013, 2015, 2016 na 2017, mawili ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, mawili ya Kombe la Tusker, manne ya Ngao ya Jamii na moja Kombe la FA. Nguli huyo pia ameiongoza Yanga kufuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika mara mbili mwaka 2016 na 2018.

Pamoja na staili yake ya kucheza soka la kutumia nguvu, Nadir ni miongoni mwa wachezaji ambao ilikuwa nadra kuadhibiwa kwa utovu wa nidhamu na mara kwa mara alionyeshwa kadi kwa rafu za kawaida mchezoni.

Akizungumza na YANGA MEDIA, Nadir alisema siri ya yeye kucheza kwa muda mrefu kwenye kiwango cha juu katika timu kubwa yenye presha kama Yanga, ni kujitunza nje ya uwanja na kuzingatia sana mazoezi.

“Siri ya kukaa muda mrefu Yanga na kucheza kwenye kiwango cha juu ni kujitunza pindi wanapokuwa nje ya uwanja na kujiepusha na mambo yanayoweza kuhatarisha vipaji vyao kama vilevi, ngono na ulaji usiokuwa na mpangilio hasa vyakula vya mafuta,” alisema Cannavaro.

Kwenye miaka 12 aliyovaa jezi ya Wananchi na Timu ya Taifa ya Tanzania, beki huyu kisiki kutoka Zanzibar amekutana na washambuliaji wengi wakali lakini kwake wanakiri waliomsumbua zaidi ni Samuel Eto’o wa Cameroon, Didier Drogba wa Ivory Coast na Haruna Moshi wa Simba.

Nadir pia amewashukuru mashabiki wa Yanga kwa upendo wao kwenye kipindi chote alichokaa Yanga, kwani Klabu hii imemsaidia sana kujenga marafiki wazuri katika maisha yake.

“Nawashukuru sana Yanga kwa kunipokea na kunilea katika kipindi chote. Kila kitu kwenye maisha yangu kimetokea Yanga. Nimejenga marafiki wengi wazuri sana pale. Najivunia sana kuwa sehemu ya historia ya Klabu yetu,” alisema Nadir.