Klabu ya Young Africans ya jijini Dar Es Salaam, leo imezindua tovuti na App rasmi ya klabu ambayo itarahisishia Wanachama,mashabiki na wapenzi wa Young Africans SC kupata taarifa,na maudhui mbalimbali kuhusiana na timu.

Uzinduzi wa tovuti na App hiyo umeambatana na uzinduzi wa awamu ya pili ya usajili wa Wanachama na mashabiki kidijitali, ambapo kwa kupitia tovuti na App. hiyo, sasa wenyewe wanaweza kujisajili kuwa wanachama au mashabiki rasmi.

Akizungumza kwenye uzinduzi huo, Rais wa Klabu ya Young Africans, Eng. Hersi Said alisema,

 “Huu ni muendelezo wa ajenda yangu kubwa katika uongozi wangu ambayo ni kuimarisha klabu kiuchumi, kupitia App na tovuti hii kunafungua mlango kwa  mashabiki na wapenzi wa Young Africans SC kuweza kujisajili kuwa shabiki au mwanachama rasmi. Hapo awali tulikuwa tunasajili kupitia fomu za karatasi na taarifa kuhifadhiwa kidijitali ila kwa sasa, utaweza kujisajili moja kwa moja kwa kupitia mifumo hii mipya. Kwa kufanya hivo,itachangia kuongeza mapato ya klabu kwa kupitia ada za usajili na uanachama zitakazotokana na mifumo hii. Ni hatua kubwa na ya kihistoria kwa klabu yetu na itasaidia sana katika kurahisisha utendaji kazi kwa ujumla.

  “Tovuti na App yetu itakuwa ikitoa taarifa na maudhui mbali mbali ambayo mashabiki wote wa Yanga wataweza kunufaika, lakini pia kurahisisha upatikanaji habari zenye usahihi kuhusiana na klabu yetu.”

Kwa upande wa Kilinet Africa ambao ndio washirika wa teknolojia wa klabu ya Young Africans, Mkurugenzi mkuu Mohamed Saleh alisema

“Hii ni awamu ya pili tulioahidi kuanzia mwanzo wa zoezi hili, ambapo sasa wapenzi wa Young Africans SC wataweza kujisajili kuwa Wanachama au mashabiki kupitia tovuti, App na USSD, kwa utaratibu huu mpya tumeshirikiana vyema na wenzetu wa Yanga na N Card ili kuhakikisha kuwa sasa watu wote watakaojisajili waweze kupata kadi zao ndani ya masaa machache. Kwa urahisi huu wa kujisajili na upatikanaji wa uhakika na haraka wa kadi za Wanachama na mashabiki, tunaamini itachangia kwa kiasi kikubwa kufikia lengo la rais wa klabu la kuiimarisha Young Africans SC kiuchumi”

Uzinduzi huo umefanyika kwenye hoteli ya Serena, jijini Dar Es Salaam mbele ya waandishi wa habari.